TUME YA MADINI

THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

MINISTRY OF MINERALS

THE MINING COMMISSION

KATIBU MKUU WA WIZARA YA MADINI AKUTANA NA MAAFISA MADINI WAKAZI WA MIKOA

Awataka kuongeza kasi katika ukusanyaji wa maduhuli, kutatua migogoro kwenye maeneo yenye uchimbaji wa madini, kudhibiti utoroshaji wa madini na kuongeza ubunifu kwenye utendaji kazi.

Dodoma

Desemba 13, 2023


Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa nchini kuongeza kasi ya ukusanyaji wa maduhuli, kutatua migogoro kwenye shughuli za uchimbaji wa madini sambamba na kuongeza kasi kwenye udhibiti wa utoroshaji wa madini ili Sekta ya Madini iendelee kuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.

Mahimbali ametoa maelekezo hayo leo jijini Dodoma kwenye kikao chake na maafisa madini wakazi wa mikoa nchini chenye lengo la kuweka mikakati ya kuimarisha Sekta ya Madini hasa katika maeneo ya ukusanyaji wa maduhuli na kuvutia uwekezaji katika Sekta ya Madini.

Amesema kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ana matarajio makubwa sana kwenye Sekta ya Madini hivyo ni vyema Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini kufanya kazi kwa bidii katika kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali za madini kupitia mapato ambayo yanatumika kuendeleza Sekta nyingine muhimu kama uboreshaji wa miundombinu, afya, elimu n.k

Amesisitiza kuwa ni vyema maafisa madini wakazi wa mikoa wakaweka nguvu kwenye ukusanyaji wa maduhuli na kuvuka lengo la makusanyo linalowekwa na Serikali kila mwaka.

Akielezea mikakati ya utatuzi wa migogoro kwenye shughuli za uchimbaji wa madini, Mahimbali amewataka maafisa madini kuhakikisha wanatatua migogoro kwenye shughuli za uchimbaji wa madini badala ya kusubiri ifikishwe katika ngazi za juu.

“Ni muhimu mkahakikisha mnatatua migogoro kwenye shughuli za uchimbaji wa madini kwa haki badala ya kukaa kimnya, na migogoro kufika ofisini kwangu, mjiamini kwa kufuata sheria ya madini na kanuni zake,” amehimiza Mahimbali.

Katika hatua nyingine, amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa kushirikiana kwa karibu na vyombo vya ulinzi na usalama kudhibiti utoroshaji wa madini na kuhakikisha vitendo vya utoroshaji wa madini havitokei katika maeneo yao ya kazi.

Pia, amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa kuendelea kubuni vyanzo vipya vya makusanyo ya maduhuli pamoja na kutangaza fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini na kuwa mstari wa mbele katika kuwasaidia wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika madini yanayochimbwa katika maeneo yao.

   

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Scroll to Top