TUME YA MADINI

THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

MINISTRY OF MINERALS

THE MINING COMMISSION

MASOKO YA MADINI YAONGEZA KASI YA MAPATO SERIKALINI

Yaingiza Shilingi bilioni 47.68 katika kipindi cha Julai – Septemba, 2023

Mikakati mipya ya udhibiti wa utoroshaji wa madini yaainishwa

Dodoma

Novemba 17, 2023

Ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inakuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi na wananchi kunufaika na rasilimali za madini, Serikali kupitia Tume ya Madini mapema Mei, 2019 ilianzisha masoko ya madini nchini kama mkakati wa kuimarisha biashara ya madini nchini.

Akielezea uanzishwaji wa masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini nchini  kwa kifupi  Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba hivi karibuni kupitia mahojiano maalum alieleza kuwa lengo la kuanzishwa kwa masoko  ya madini lilikuwa ni kuhakikisha wachimbaji wa madini wanafanya biashara ya uhakika huku Serikali ikikusanya kodi mbalimbali na kufungua fursa za ajira sambamba na kudhibiti vitendo vya utoroshaji wa madini.

“Ikumbukwe kuwa kabla ya kuanzishwa kwa masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini nchini, wachimbaji wadogo wa madini walikuwa hawana soko la uhakika la madini yao, na wakati mwingine walikuwa wanauza madini yao kwa bei ya hasara kutokana na kutokuwepo kwa bei elekezi ya madini hayo na wanunuzi wa uhakika,” alisema Mhandisi Samamba.

Soko la Madini Geita

Aliendelea kusema kuwa hadi kufikia Septemba, 2023, jumla ya Masoko 42 na vituo vya ununuzi wa madini 95 vilikuwa vimeanzishwa nchini ambapo Tume ya Madini imeendelea kusimamia biashara ya madini katika masoko hayo ili kuhakikisha yanafanya kazi kwa ufanisi.

Akielezea utendaji wa masoko ya madini kwa kipindi cha robo mwaka wa fedha 2023-2024, Mhandisi Samamba alisema kuwa katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Septemba, 2023 kiasi cha tani 4.87 za madini ya dhahabu, tani 106.29 za madini ya Bati, karati 1,550.76 za madini ya Almasi, karati 7,893.85 na tani 18.95 za madini ya tanzanite na kiasi cha karati 35,545.14 na tani 15,946.11 za madini mengine ya vito yaliuzwa katika masoko ya madini.

Alisema kuwa mauzo ya madini hayo yamechangia makusanyo (mrabaha na ada ya ukaguzi) kiasi cha Shilingi bilioni 47.68 ambapo kati ya fedha hizo, kiasi cha Shilingi bilioni 40.52 zilitokana na mrabaha na Shilingi bilioni 7.16 zilitokana na ada ya ukaguzi.

Aliendelea kusema kuwa  kiasi hicho cha makusanyo ya Shilingi bilioni 47.68 kwa robo ya kwanza ya mwaka 2023/2024 ni ongezeko la makusanyo ya Shilingi bilioni 6.91 ukilinganisha na makusanyo ya Shilingi bilioni 40.77 kwa kipindi kama hicho kwa mwaka 2022/2023.

Mhandisi Samamba aliongeza kuwa katika kipindi husika yalifanyika mauzo ya dhahabu yenye uzito wa tani 4.87 yenye thamani ya Shilingi bilioni 659.00 kupitia masoko ya madini yaliyoiwezesha Serikali kupata mapato kutokana na mrabaha na ada ya ukaguzi kiasi cha Shilingi bilioni 45.81.

Akielezea manufaa mengine yaliyopatikana kutokana na uanzishwaji wa masoko ya madini na vituo  vya ununuzi wa madini, Mhandisi Samamba alisema kuwa yamezalisha ajira zaidi sambamba na kupunguza kwa kiasi kikubwa vitendo vya utoroshaji wa madini.

Wakati huohuo akielezea mikakati iliyowekwa na Tume ya udhibiti wa utoroshaji wa madini nchini, Mhandisi Samamba alieleza kuwa Tume kupitia Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na vyombo vya ulinzi na usalama katika udhibiti wa vitendo vya utoroshaji wa madini nchini.

Alieleza mikakati mingine kuwa ni pamoja na kuwepo kwa wakaguzi wa madini katika maeneo yote ya bandari, viwanja vya ndege na mipakani na kuongeza kuwa watuhumiwa wote wanaokamatwa wakitorosha madini wamekuwa wakifikishwa katika vyombo vya sheria kwa hatua stahiki.

Aliongeza kuwa pia Tume imekuwa ikitoa elimu ya uzalendo kwa wadau wote wa sekta ya madini juu ya athari zitokanazo na utoroshaji wa  madini. Baadhi ya athari hizo ni uhujumu uchumi wa nchi na kukosesha ajira kwa watanzania.

“Ni kosa kubwa kushiriki katika vitendo vya utoroshaji wa madini ambapo ukipatikana na hatia madini yanataifishwa, kufutiwa leseni zote za madini ambapo hutaweza kufanya shughuli yote ya madini nchini na kufungwa jela,” alisisitiza Mhandisi Samamba.

Wakati huo huo Mhandisi Samamba aliwataka wadau wa madini kufuata Sheria ya Madini, kanuni zake na miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali na kusisitiza kuwa Tume ya Madini itaendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili Sekta ya Madini.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *