TUME YA MADINI

THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

MINISTRY OF MINERALS

THE MINING COMMISSION

TUME YA MADINI YAJIVUNIA MAFANIKIO MAKUBWA

Ikiwa ni utekelezaji wa kanuni za ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini

Asilimia 86 ya kampuni za wazawa zinatoa huduma na bidhaa migodini huku asilimia 14 zikitolewa na kampuni za nje ya nchi kupitia kibali maalum kinachotolewa na Tume ya Madini

Ajira katika migodi ya madini asilimia 97 ni watanzania huku raia wa kigeni wakiwa ni asilimia tatu

 

Dodoma

 

Desemba 01, 2023

 

Ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inakuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi na wananchi kunufaika na rasilimali za madini, Serikali kupitia Tume ya Madini ilifanya maboresho mbalimbali ya Sheria ya Madini na kanuni zake yenye lengo la kuhakikisha kunakuwepo na ongezeko la ushiriki wa watanzania katika Sekta ya Madini na Serikali kupata kodi mbalimbali sambamba na kuzalisha ajira zaidi.

Moja ya maboresho ni pamoja na kutungwa kwa kanuni za ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini (Local Content) ambazo zimeleta manufaa kwa wadau wa madini hususan wananchi wanaoishi jirani na migodi ya madini.

Tume ya Madini ina jukumu la kusimamia ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini ili kuhakikisha Watanzania wananufaika na fursa zilizopo katika Sekta ya Madini pamoja na kufungamanisha Sekta ya madini na Sekta nyingine za kiuchumi.

Akielezea uanzishwaji wa kanuni hizo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba hivi karibuni kupitia mahojiano maalum alieleza kuwa lengo la kuanzishwa kwake lilikuwa ni kuongeza ushiriki wa watanzania katika Sekta ya Madini kuanzia kwenye shughuli za utafutaji wa madini, uchimbaji wa madini, masoko ya madini sambamba na kutoa huduma kwenye migodi ya madini kama vile ajira, ulinzi na vyakula.

Aliendelea kusema kuwa lengo lingine lilikuwa ni kuhakikisha kampuni za uchimbaji wa madini zinatumia bidhaa zinazozalishwa nchini badala ya kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi hivyo kuwezesha wananchi kujipatia kipato huku Serikali ikipata kodi mbalimbali.

Akielezea manufaa yaliyopatikana tangu kuanzishwa na utekelezaji wa kanuni husika, Mhandisi Samamba alisema kuwa mpaka sasa asilimia 86 ya kampuni za wazawa zinatoa huduma na bidhaa migodini huku asilimia 14 zikitolewa na kampuni za nje ya nchi kupitia kibali maalum kinachotolewa na Tume ya Madini na kwa upande wa ajira katika migodi ya madini asilimia 97 ni watanzania huku raia wa kigeni wakiwa ni asilimia (3) tatu.

“Ieleweke kuwa hakuna kampuni yoyote inayoruhusiwa kuagiza bidhaa au huduma kutoka nje ya nchi bila kupata kibali kutoka Tume ya Madini, lengo letu ni kuhakikisha kila mtanzania ananufaika na Sekta ya Madini,” alisema  Mhandisi Samamba.

Aliongeza kuwa katika usimamizi wa kanuni za ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini, Tume ya Madini kupitia Kamati ya Ushirikishwaji wa Watanzania, imeendelea na jukumu lake la msingi la kuchambua mipango inayowasilishwa na kampuni zote zinazojishughulisha na uchimbaji na utafutaji wa madini pamoja na watoa huduma katika Sekta ya Madini kama takwa la Sheria ya Madini ya mwaka 2010 pamoja na marekebisho ya mwaka 2017 na Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania za Mwaka 2018 pamoja na maboresho yake.

Akielezea utekelezaji wake katika kipindi cha robo ya mwaka wa Fedha 2023/2024 Mhandisi  Samamba alisema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba, 2023 Tume ya Madini ilipokea jumla ya mipango 234 ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini iliyowasilishwa katika kikao cha Kamati ya Ushirikishwaji wa Watanzania kwa ajili ya kupitishwa. Mipango yote 234 iliwasilishwa kwa mara ya kwanza kwa ajili ya kufanyiwa uchambuzi na kuidhinishwa kwa mujibu wa Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania.

“Kati ya Kampuni 234 zilizowasilisha maombi mapya ya kuidhinishiwa mipango ya Ushirikishwaji wa Watanzania, kampuni tatu zinamiliki leseni ya Uchimbaji Mkubwa, Kampuni tano zinamiliki/zinaomba leseni za Uchimbaji wa Kati, Kampuni saba  zinamiliki/zinaomba leseni ya Utafti  na kampuni 219 ni za watoa huduma mbalimbali (Contractors & Sub-contractors) kwa wamiliki wa leseni za madini,” alisema Mhandisi Samamba.

 

Akielezea mikakati iliyowekwa na Tume katika kuhakikisha watanzania wengi wanashiriki kwenye Sekta ya Madini Mhandisi Samamba alieleza kuwa ni pamoja na kutoa elimu kwa kampuni zinazomiliki leseni za madini pamoja na kuandaa Majukwaa na Warsha mbalimbali kuhusu utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini na kushiriki maonesho mbalimbali yanayohusu teknolojia ya Madini na kutoa elimu kwa washiriki.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Scroll to Top