TUME YA MADINI

THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

MINISTRY OF MINERALS

THE MINING COMMISSION

WANAWAKE NA MADINI

SERIKALI YAWATAKA WANAWAKE NJOMBE KUCHANGAMKIA FURSA ZA UCHIMBAJI MADINI

Na Mwandishi Wetu, Njombe

Kufuatia mkoa wa Njombe kuwa na hazina kubwa ya aina mbalimbali za madini, Serikali imewataka wachimbaji wadogo wa madini wanawake mkoani Njombe kuchangamkia fursa za uchimbaji wa madini ili waweze kujikwamua kiuchumi pamoja na familia zao.

Rai hiyo imetolewa leo mkoani Njombe na  Nerasi Mulungu ambaye ni Afisa Elimu Mkoa kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Njombe, Judica Omari wakati akifungua mafunzo ya mnyororo wa sekta ya madini ikiwa ni pamoja na fursa za uwekezaji zilizopo yaliyoshirikisha wajasiriamali, wadau na wachimbaji wadogo wa madini wanawake.

Nerasi amesema  kuwa anafahamu wanawake wa mkoa wa Njombe ni wachapakazi katika kujitafutia maendeleo ya kiuchumi, na kusisitiza kuwa wanayo fursa nzuri ya kugeukia uchimbaji wa madini ambao umekuwa ukisaidia kukuza uchumi.

“Lengo la mafunzo haya ni kujengeana uwezo, kuelimishana kuhusu uendeshaji wa shughuli za madini kwa upande wa wanawake, hii ni fursa ya kipekee naomba wanawake mliopata fursa hiyo muwe mabalozi kutangaza hizi fursa za uchimbaji wa madini kwa wanawake, mara nyingi tunaposema fursa za uchimbaji wa madini wanawake wengi wanajikuta wanapata fursa za kuwa mama lishe kwenye sehemu za madini, lakini hapa nimefurahi kuna wanawake  wadogo wanaojishughulisha na  uchimbaji wa madini kwa hiyo tuongezeke tuwe wengi,” amesema Nerasi.

 Amesema kuwa,  kila mwanamke ambaye ameshiriki mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Njombe anao wajibu wa kutumia fursa hiyo kuchangamkia biashara ya uchimbaji wa madini kwa kuwa umesaidia kuleta mabadiliko chanya kwa wanawake mbalimbali nchini.

Kwa upande wake Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Njombe, Zabibu Napacho akizungumzia lengo la kuwakutanisha wanawake wachimbaji wadogo wa madini mkoani Njombe amesema kuwa wameamua kufanya mafunzo hayo kwa kuwa wanawake wengi mkoani humo hawajihusishi katika shughuli za uchimbaji wa madini.

“Wanawake wengi hawana uelewa wa uchimbaji wa madini hivyo wamekuwa na hofu ya kujihusisha na shughuli nzima za uchimbaji wa madini kwa hiyo tulikuwa katika makongamano mbalimbali na walitoa maoni yao kuwa wanahitaji kupata uelewa ili waweze  wenyewe kuingia katika shughuli za madini,” amesema Zabibu.

Naye mwenyekiti wa chama cha wachimbaji wa madini tawi la Njombe, Judith Sanga amesema kuwa mkoa wa Njombe unaongoza sana kwa madini ya viwandani na hivyo wanachokihitaji kwa sasa ni vitendea kazi vya uchimbaji kwa kuwa machimbo mengi ya madini mkoani humo yanahitaji vitendea kazi.

Baadhi ya wanawake wanaopatiwa mafunzo hayo akiwemo Katibu wa Kikundi cha Wanawake Wachimbaji Madini Samia (NJOWAMA), Saada Msangi amesema kuwa mafunzo hayo kwao yana tija sana kwa kuwa wanawake wa mkoa wa Njombe wameanza kuhamasika kwa kutambua kuwa madini ni maisha na utajiri hivyo hawapaswi kujifunga, kuwa na malalamiko au kutokufanya kazi kwa bidii.

 

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Scroll to Top